click here

click here

UONGOZI WA UKEREWE WAZUIA WAKULIMA KULIMA MILIMANI

UONGOZI WA UKEREWE WAZUIA WAKULIMA KULIMA MILIMANI


Na Queen Ndosi

Katibu Tawala wa Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza, Focas Majumbi amepiga marufuku kilimo cha milimani ili kuukabili uharibifu wa mazingira unaosababishwa na kilimo hicho na mabadiliko ya tabia Nchi.

Akizungumza na wakulima wa bonde la Miyogwezi lililoko kijiji cha Igongo jana, Majumbi alisema milima hiyo ikiachwa itarejea kwenye uoto wa asili na kuvutia mvua zitakazowezesha kupata mazao ya kutosha.

Akifafanua, alisema kwa miaka ya hivi karibuni Wilaya hiyo inaendelea kukabiliwa na upungufu wa chakula kwa sababu ya uhaba wa mvua, hivyo amezitaka serikali za vijiji kusimamia kikamilifu agizo hilo. Alisema hatakuwa tayari kuona milima na misitu ikifyekwa bila utaratibu, huku linapotokea tatizo kama la upungufu wa chakula serikali inalaumiwa kwa sababu ya matatizo yanayosababishwa na baadhi ya watu kwa manufaa
binafsi.

Awali Katibu wa kikundi cha wakulima wa bonde la Miyogwezi, Marco Matto alisema wakulima 196 wanategemea mradi huo ulioanza kujengwa mwaka 2002 kuendesha maisha yao lakini hadi sasa haujakamilika.

Hatahivyo, alisema pamoja na shirika la Maendeleo la Japan (JICA) kuwajengea uwezo na kuwapa mbegu bora za kisasa za mpunga aina ya TXD 306 na SARO 5, lakini wameshindwa kufikia malengo yao kwa sababu miundombinu ya hekta 120 za mradi huo wa umwagiliaji haijakamilika.

Wakithibitisha tatizo hilo, wakulima hao wamesema wanakatishwa tamaa na mipango ya serikali katika kukakamilisha mradi huo ambao ungepunguza tatizo la upungufu wa chakula. Naye Alex Mugaya alisema mbali ya mradi huo kuchukua muda mrefu, pia wanahitaji pembejeo za kilimo kama trekta na mashine za kupandia na kuvuna mazao ili kukidhi mbinu na mafunzo waliyopata.

Ofisa Kilimo na Ushirika wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, Ibrahimu Samson alisema mradi uliokuwa ukitekelezwa na DASP ulikwama baada ya shughuli za mfadhili kumalizika na tayari taarifa hizo zimefikishwa ngazi husika.

No comments

Powered by Blogger.