Maalim Seif azungumza juu ya kitendo cha JPM kumteua Anna Mghwila kuwa Mkuu wa Mkoa.
Maalim Seif azungumza juu ya kitendo cha JPM kumteua Anna Mghilwa kuwa Mkuu wa Mkoa.
Na Ulwe Rajab
Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad
amemkingia kifua Rais Dk. John Magufuli kwa uamuzi wake wa kumteua
Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo, Anna Mghwila kuwa Mkuu wa Mkoa wa
Kilimanjaro.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam, Maalim Seif
alisema Rais Magufuli hajakosea kwa uteuzi huo kwa kuwa hapangiwi nani
amuweke wapi na nani asimuweke.
“Uteuzi ni haki yake, wala hatuingilii maamuzi yake kwa sababu kuteua au
kutoteua ni yeye na kuteua ACT na kuacha vyama vingine huenda yeye
mwenyewe ana yake moyoni na kwamba hajaamua kufanya hivyo.
“Mimi sikuingia katika moyo wake na kwa kufanya hivyo si jambo geni kwa
kuwa wapo waliopita waliwapa wapinzani ubunge, lakini pia ni Rais wa
kwanza kuingiza mtu wa chama kingine kwenye serikali katika utendaji…si
jambo baya kwa maana linaweza jenga upya Serikali,’’ alisema.
Alisema Rais Magufuli ametumia mfumo ambao pia hutumiwa na nchi za Bara
la Ulaya na Marekani, ambapo Rais Mstaafu wa Marekani, Barack Obama naye
aliutumia.
“Siwezi kushangaa kwani inaweza ikatokea siku akamteua Naibu Katibu Mkuu
wangu, Joran Bashange kuwa Waziri wa Nishati na Madini,” alisema Maalim
Seif huku waandishi na maofisa wa chama hicho wakiangua kicheko.
UVCCM
Nao Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), umesema hatua ya
Rais Dk. Magufuli kumteua Anna Mghwira kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro
ni kitendo cha kijasiri na cha kizalendo kwa sababu hakuna alipokosea.
Pamoja na hali hiyo, umoja huo umesema uteuzi wa nafasi ya RC Mghwira,
ni wazi ataisimamia na kuongoza kwa hekima, busara na uzalendo kwa
masilahi ya Taifa.
Kauli hiyo, imetolewa Dar es Salaam jana na Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka.
Alisema uteuzi huo, usiibue nongwa na kuonekana kuna jambo limekosewa.
Pamoja na hali hiyo Shaka, alisema Katiba ya nchi hairuhusu mgombea
binafsi na kwamba kila mgombea urais, udiwani au ubunge hutokana na
chama cha siasa ila anaposhinda urais huwa na mamlaka ya kuteua mtu
yeyote ili mradi awe Mtanzania bila ubia.
Alisema Rais Dk. Magufuli, ana haki na wajibu wa kumteua mtu yeyote
atakayeona anafaa kushika nafasi atakayomteua ilimradi aliyeteuliwa awe
ana hisia za uchapakazi, mpenda umoja na mzalendo.
Shaka alisema katiba ya CCM imetamka ikiwa kutakuwa na mkuu wa mkoa
anayetokana na CCM atashiriki vikao vya Kamati ya Siasa ya Mkoa wakati
wa vikao lakini kwa suala la Mghwira lipo tofauti kwani anatokana na
chama kingine na ikiwa ataona kuna haja ya kujiunga na CCM basi naye
atapata fursa ya kushiriki vikao hivyo.
“Ila kwa sasa hasa baada ya kuripoti katika eneo lake la kazi hatoweza
kuhudhuria vikao vya Kamati ya Siasa ya Mkoa kwa kuwa si mwana CCM ila
kama ataona kuna haja ya kujiunga na CCM hazuiwi na atakuwa na haki ya
kuhudhuria vikao vyote.
“Kwa hili Rais Dk. Magufuli anabaki kuwa nembo ya demokrasia ya kweli
nchini kwetu kwa kushirikisha wapinzani kwenye nafasi nyeti za utendaji.
“Viongozi wa Serikali wakiteuliwa hula viapo vya utii ambavyo
vimeandikwa kisheria katika medani za uendeshaji Serikali, mteule wa
Rais hali kiapo cha kisiasa bali huapa kiapo cha kutumikia nchi na watu
wake kwa mujibu wa sheria za nchi na Katiba,” alisema Shaka.

Post a Comment