Lowassa,Mbowe na Sumaye waonesha hisia zao juu ya Demokrasia mbele ya Jeneza la Ndesamburo
Waliokuwa Mawaziri wakuu wastaafu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye jana
walitema cheche katika shughuli ya kuaga mwili wa mbunge wa zamani wa
Moshi Mjini (Chadema), Philemon Ndesamburo.
Mawaziri hao katika salamu zao za rambirambi walielezea masikitiko yao
juu ya chuki kubwa inayopandikizwa nchini na pia jitihada zinazoendelea
za kukandamiza demokrasia.
Hata hivyo, hakuna kiongozi yeyote wa Serikali aliyehudhuria shughuli
hiyo hali ambayo ilionekana kuibua minong’ono kwa baadhi ya
waombolezaji.
Mwenyekiti mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), James Mbatia
alienda mbali zaidi na kusema hakukuwa na uwakilishi wa CCM unaofanana
na sifa ya Ndesamburo aliyependa amani.
Katika hafla hiyo ya kumuaga kitaifa iliyofanyika uwanja wa Majengo,
wabunge wa CCM waliwakilishwa na mbunge wa viti maalumu, Ester Mmasi
aliyedai kuiwakilisha pia CCM.
Hotuba ya Mbowe
Hotuba ambayo iligusa hisia za waombolezaji wengi ni ya mwenyekiti wa
Chadema, Freeman Mbowe aliyesema hatua ya viongozi wa Serikali na CCM
kutohudhuria si tukio la bahati mbaya.
“Leo tumejenga Taifa lenye hofu. Watu wamekuwa waoga kwa sababu viongozi
wameingiza hofu katika Taifa letu. Watu wenye hatia wana hofu.
Kukosekana kwa uwakilishi wa Serikali mahali hapa si ajabu,” alisema
Mbowe na kuongeza:
“Ni hofu ya hatia. Kwa heshima sana dada yangu Mmasi (Ester) pole.
Asante sana kwa kufika. Umekuja hapa na kujaribu sana unamwakilisha
sijui Serikali, sijui Rais. Hakuna.”
Mbowe alisema ameona vituko vingi katika msiba wa Ndesamburo kiasi
kwamba anajiuliza inakuwaje wakati alikuwa mtu mwema na walitamani hata
kumsindikiza kwa bendi ya polisi. “Tukaenda Chuo cha Polisi kuomba bendi
ambacho mzee (Ndesamburo) anawasaidia mambo mbalimbali. Brass band hii
inakodishwa kwa Sh300,000, tulikuwa tayari kulipa gharama hiyo,” alisema
Mbowe na kuongeza:
“Mkuu wa chuo anaogopa kutoa Brass band ananiambia mwenyekiti Mbowe
ongea na IGP (mkuu wa Jeshi la Polisi). Yaani Mbowe nimpigie IGP simu
kumuomba Brass band (bendi ya polisi), mimi?”
“Leo polisi wanaogopa kufanya kazi kwa sababu hawajui bwana mkubwa
atafurahi ama atakasirika. Ni mambo ambayo si ya Kitanzania. Tukahitaji
kiwanja cha kumuaga baba nacho tukanyimwa.”
“Si kwamba kiwanja hiki cha Majengo hakifai. Ila kwa historia ya Moshi,
uwanja wa Mashujaa kama unavyoitwa unastahili kuwa uwanja wa kuagwa mzee
wetu Ndesamburo. Polisi wakaweka mizengwe.”
Mbowe alisema alifanya juhudi kubwa ikiwamo kuwasiliana na Waziri Mkuu,
Kassim Majaliwa ambaye alimueleza kuwa anashughulikia, lakini hata hivyo
ilikuwa ahadi hewa.
“Tulisema baba yetu ni kiongozi wa watu na sio wote wataweza kuja
uwanjani. Tukaona ni haki tumpitishe (Ndesamburo) katikati ya mji lakini
usiku tukaletewa barua ya zuio la polisi,” alisema.
“Kuna kiburi kinajengwa sana mikoa ya Kilimanjaro na Arusha. Naomba
nimpelekee salamu mheshimiwa Rais, Watanzania wote sisi ni ndugu,”
alisisitiza Mbowe ambaye ni mbunge wa Hai.
“Mwalimu (Nyerere) alitujenga tukawa tunapendana, lakini utawala huu wa
awamu ya tano unafanya matendo yanayoonyesha ubaguzi na tunaona uonevu
usiohimilika kwa mikoa ya Kilimanjaro na Arusha”.
Mbowe alisema ingawa watu wengi wanaogopa kuyasema hayo, yeye atayasema
ili Rais, Waziri Mkuu na Serikali nzima ielewe kuwa Kilimanjaro na
Arusha ni sehemu ya Tanzania.
“Watu wengi wanaogopa kusema. Siku hizi hata unaogopa kusema wewe ni
Mushi. Uongo? Siku hizi watu wanaogopa kujiita Masawe, kujiita Tarimo
kwa sababu huna uhakika watawala watafanya nini.”
“Hatuhitaji kujenga Taifa lenye ubaguzi, tunahitaji kumheshimu na
kumthamini kila Mtanzania bila kujali dini yake, kabila lake wala
jinsia. Tumuenzi Ndesamburo kwa kupendana,” alisema Mbowe.
Mbowe alisema Ndesamburo katika uhai wake alifanya mambo mengi na
alikuwa mfadhili mkubwa si kwa Chadema pekee, bali watu wengi na makundi
mbalimbali.
“Wakati polisi wanakuja kutufukuza katika uwanja wa Mashujaa na mabomu.
Tukawaambia gari mnaloendesha tairi amenunua Ndesamburo. Na ni ukweli,
sio nasema maneno ya uongo.”
“Huyu baba amejenga Mawenzi (hospitali) nani asiyejua. Amesaidia taasisi
mbalimbali za dini, Wakristo na Waislamu. Amesaidia mashule sio tu kwa
mkoa wa Kilimanjaro hata mikoa mingine.”
Mbowe alisema pamoja na kujitoa kwake huko, wako watu wanashindwa kuona
thamani yake kwa sababu ya itikadi za kisiasa na kusisitiza kuwa siasa
ni mambo ya mpito, lakini jamii itabaki.
“Leo sisi tunazika huku, bungeni wanamsimamisha Halima Mdee na Ester
Bulaya. Hatuwezi kujenga Bunge la vibogoyo. Hatuwezi kujenga Bunge la
wabunge waoga,” alisisitiza kiongozi huyo wa upinzani.
“Hii nchi imefika hapa kwa sababu kuna watu waoga na wenye hofu. Ugomvi
wa Ester Bulaya na Halima Mdee ulianza wakati wa bajeti ya Nishati na
Madini.”
“Katika mjadala ule mheshimiwa Mnyika (John) kaamriwa kutoka nje na
spika kwa uonevu ulio dhahiri. Wabunge wale akina mama wakasimama
wakasema huyu mtu hatendewi haki. Wabunge msifungwe midomo na mkienda
bungeni wabunge wote msimame imara na Watanzania bila kujali vyama vya
siasa tuitake nchi hii ijifunze kuhoji viongozi wanapofanya makosa.”
Mbowe alitumia hadhara hiyo kutuma salamu kwa wale aliosema wanafikiri
kuondoka kwa Ndesamburo ni kuterereka kwa Chadema akisema haitatokea na
wataendelea kuijenga vyema Moshi.
Sumaye, Lowassa na Mbatia
Sumaye ambaye ndiye aliyeongea kwa kirefu alisema Afrika itaendelea kama
Serikali zilizo madarakani zitaenzi demokrasia na kuachia madaraka kwa
amani badala ya kung’ang’ania.
“Kuna juhudi kubwa sana zinaendelea za watu kujidanganya kuwa wanaweza
kukandamiza demokrasia. Hapa demokrasia ilipofikia huwezi tena
kuikandamiza,” alisema Sumaye na kuongeza:
“Mpira una bladder (puto) ndani. Ukiikandamiza sana itapasuka na
ikipasuka itakuwa na madhara makubwa. Tuache Watanzania wafurahie
demokrasia katika nchi yao. Hili ni muhimu.”
“Tuache kupandikiza chuki. Mikutano ya siasa inazuiwa, njia za kupitisha
maiti (ya Ndesamburo) zinazuiwa. Hatuwezi kuwaonea wananchi hawa kwa
muda mrefu.”
Lowassa aliunga mkono maneno yaliyosemwa na Sumaye kuhusu jitihada kubwa
zinazoendelea za kudidimiza demokrasia na kupandikiza chuki katika
jamii.
“Jitihada za kudidimiza demokrasia inaendelea sana. Hawa waliozuia
tusiagie Mashujaa tuwasamehe. Hupimi watu kwa uwanja, bali kwa roho
zao,” alisema Lowassa aliyegombea urais mwaka 2015 kupitia Ukawa.
Awali, katika hotuba yake Mbatia alilaani tabia iliyoanza kujengeka ya
kuwafarakanisha Watanzania na kumtaka Rais Magufuli ajue kuwa Tanzania
ni ya Watanzania wote.
Mbatia ambaye pia ni mbunge wa Vunjo (NCCR-Mageuzi) alitoa mfano wa
tukio la Aprili 30, wakati Rais alipofanya ziara mkoani Kilimanjaro
ambapo meya na mbunge walitimuliwa Ikulu.
“Mbunge wa Moshi Mjini (Jaffar Michael) na meya wa Moshi (Raymond Mboya)
wakaondolewa Ikulu na Rais akakaa kimya tu. Tanzania ni mali ya
Watanzania na sio ya John Pombe Magufuli,” alisema.
“Tangu tumeanzisha mageuzi haya labda John Magufuli alikuwa shule,
lakini hatuwezi kukubali Taifa letu likasambaratika kwa maslahi ya watu
wachache,” aliongeza kusema na kusisitiza:
“Rais akija Moshi, mwenyeji wako ni meya na mbunge, watu wako wa usalama hawawezi kuwaondoa.
“Niwaombe CCM, Tanzania ni mali ya Watanzania wote, nitaongea nao.
Kitendo walichofanya leo sio utamaduni wa Watanzania. Sioni uwakilishi
wa CCM unaofanana na Ndesamburo.”
Makamu Mwenyekiti wa CUF, Severina Mwijage alisema wale wote waliozuia
Ndesamburo asiagwe katika Uwanja wa Mashujaa Mungu atawalipa kwa kile
walichokifanya.
“Huwezi kuwachonganisha wananchi namna hii. Chadema mna salamu inasema
peoples power. Tungeamua kutumia nguvu ya umma msingeweza (polisi)
kufanya lolote,” alisema.
Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe alipendekeza halmashauri ya
manispaa ya Moshi inayoongozwa na Chadema kutafuta mtaa bora ndani ya
mji na upewe jina la Ndesamburo.
Zitto alisema hiyo itakuwa ni njia bora ya kuenzi mchango mkubwa wa
Ndesamburo katika jimbo hilo ili mtu yeyote akifika Moshi ajue jabali la
siasa alikuwa anaishi mjini humo.
Katika shughuli hiyo ya kuaga mwili wa Ndesamburo, waziri wa zamani wa
fedha na mbunge wa zamani wa Rombo (CCM), Basil Mramba alikuwa kivutio
alipoingia uwanjani hapo.

Post a Comment