Chadema wamtwika Sirro Sakata la Kupotea Ben Saanane
Chadema wamtwika Sirro Sakata la Kupotea Ben Saanane
Simon Sirro ambaye ni Mkuu wa Jeshi la Polisi, ametakiwa kutoa tamko juu ya kupotea kwa Mkuu wa Idara ya Sera na Utafiti wa Chadema, Ben
Saanane, ambaye alipotea tangu Novemba
18, mwaka jana katika mazingira ya kutatanisha.
Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema
(Bavicha), Patrobas Katambi katika mkutano wake na Waandishi wa Habari
uliofanyika Makao Makuu ya chama hicho, Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Katambi ambaye alizungumzia kuhusu vitendo vya utekaji, ubambikaji kesi
na uvunjaji wa haki za binadamu, alisema Jeshi la Polisi liko kimya juu
ya taarifa za wapi alipo Saanane.
“Mnakumbuka majibu ya Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) alipoulizwa kuhusu
alipo Ben alitafuna maneno, hali iliyoonyesha anajua nini kinaendelea
kuhusu Ben. Bavicha tunamtaka IGP mpya Sirro kutoa kauli ya Jeshi la
Polisi kuhusu wapi aliko Ben, hasa kwa kuwa aliahidi kuwa vitendo vya
kihalifu vitakoma na tunamtaka aanze na hili la Ben,” alisema.
Katambi pia alisema IGP Sirro anapaswa kubadili mfumo wa utendaji wa
jeshi hilo, ili kuondoa uonevu dhidi ya raia, kuminya uhuru wa maoni,
kukamata na kubambikia kesi raia wasio na hatia.
Alisema vijana wengi wanadhalilika kwa kukamatwa, hasa wa Chadema na
kwamba katika mwendelezo huo, hata Yeriko Nyerere alikamatwa na watu
wasiojulikana.
Katambi alisema yeye mwenyewe aliwahi kutekwa na watu wasiojulikana mara
mbili, ikiwapo mwaka wa Uchaguzi Mkuu 2015, hivyo anashindwa kuelewa
hadi imtokee nani ndipo hatua zichukuliwe.
“Tunazungumza ili hatua stahiki zichukuliwe, ikishindikana tutachukua
hatua na sheria mikononi kumtafuta Ben Saanane,” alisema Katambi.
Akizungumzi suala la kutolewa silaha hadharani, alisema limeshawatokea
baadhi ya viongozi waliokuwa serikalini, hivyo IGP Sirro ana wajibu
mkubwa wa kusimamia utawala wa sheria.

Post a Comment